Monday, August 17, 2015

MABASI YAENDAYO KASI YAZINDULIWA TANZANIA


Leo jiji la Dar es Salaam limeshuhudia uzinduzi wa huduma ya mpito (Interim Services) ya mradi wa mabasi ya haraka Bus Rapid Transport (BRT).
Mradi huu wa mabasi yaendayo haraka unaozinduliwa leo utaandika historia ya kuliweka jiji la Dar es Salaam kuwa jiji lapili barani Afrika kutekeleza mradi huu likitanguliwa na jiji la Capetown la nchini Afrika Kusini.
Kampuni ya ubia ya UDA Rapid Transport (UDART) kwa kushirikiana na Wakala wa Mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaa (DART) utaanza leo kuendesha mafunzo kwa madereva kabla ya usafiri huo kuanza rasmi Oktoba mwaka huu. 
Ujio wa mabasi hayo yenye uwezo wa kubeba watu 190 na mengine watu 100 ni mwanzo wa mwisho wa matumizi ya mabasi maarufu ya daladala katika njia ya Kimara hadi Kivukoni. Kwa kuanzia tayari kuna mabasi 76 yatakayoanza kuhudumu rasmi ifikapo Oktoba mwaka huu na mengine yako njiani kuingizwa nchini kwa ajili hiyo. 
Mabasi hayo yatatumia dakika 20 pekee kwa safari ya kutoka Kimara hadi Kivukoni safari ambayo kwa usafiri wa daladala za kawaida hutumia hadi zaidi ya saa 2 kwa umbali huo. 
Mabasi haya ndani yana viti maalumu kwa ajili ya wazee, wajawazito na wenye ulemavu. Yana mikanda maalum ya kushika abiri wanaosimama na hayatakuwa na makondakta wala wapiga debe kwa kuwa nauli hazilipwi ndani ya basi bali hulipwa kituoni kabla abiria hajapanda ndani ya basi. 

Kufanikisha shamrashamra hizo leo wakazi wa Dar watapata fursa ya kupanda bure kwa siku ya leo mabasi haya kutoka kituo cha Ubungo kwenda Kimara na kurudi hadi kituo cha Kivukoni. 
Ni budi pia kutoa tahadhari kwa sisi wananchi ambao tutakuwa watumiaji wa mradi huu kuwa makini na kuulinda mradi huu na miundombinu yake ili utupe huduma yenye ufanisi. Ni masikitiko baadhi ya watu wamekuwa wakiharibu miundombinu ya vituo kwa kuiba vifaa, wengine wanakusudia kuiba milango na madirisha ya vioo yaliyowekwa vituoni, wako wanaoharibu kwa kuzigonga nguzo zilizowekwa kuzuia au kurahisisha matumizi ya miundombinu hii. Madereva wa magari na bodaboda hawaruhusiwi kuzitumia njia maalumu za mabasi haya ingawa baadhi yao wameapa kuwa hawatoacha. 





No comments:

Post a Comment