
Hatimaye marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wameungana na wajumbe wenzao wa Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza kuwajadili makada waliojitokeza kuwania urais na kutoa ushauri utakaowezesha kupatikana kwa njia bora za kumpata mgombea wa chama hicho.
Tayari vikao vya baraza hilo vilivyokuwa vikisubiriwa kwa hamu vimeshaanza na leo vinaingia katika siku yake ya tatu, kwenye ofisi moja nyeti jijini Dar es Salaam.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya baraza la wazee hao zinaarifu kuwa vikao hivyo vina umuhimu wa pekee katika mchakato huo na kwamba vimepewa eneo tulivu na lenye usalama wa hali ya juu.
"Kikao kimeanza hapa (anataja ofisi) tangu juzi (Jumamosi) na hivi sasa bado tunaendelea,” kilieleza chanzo kimoja toka ndani ya kikao hicho.
Katika hali inayoonyesha umuhimu wa ushauri wa baraza hilo, chanzo hicho kinasema, “tuombe Mungu ili yanayoazimiwa na wazee wetu yakamilike na kuweza kukipa sura mpya chama chetu (CCM).”
No comments:
Post a Comment